Monday, March 08, 2010

TANZANITE SOCIETY JP

Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Japani - Tanzanite jana ilikuwa na mkutano wake ambako mada mbalimbali zilijadiliwa. Mkutano huo uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa Jumuiya, Dr. Ally Y. Simba uliwasilisha mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mkuu kwa ajili ya viongozi wapya wa Jumuiya. Wajumbe wa mkutano huo waliridhia vigezo vilivyopendekezwa na uongozi vitakavyotumika kwa wale wanaotaka kuwania nafasi za uongozi kujipima. Aidha mkutano huo pia ulijadili suala la vurugu zilizojitokeza hivi karibuni na kutoa taarifa ya juhudi za usuluhishi na adhabu zilizotolewa kwa wale waliochochea vurugu hizo. Viongozi na wajumbe wote walikubaliana kuwa kuna umuhimu wa kujaribu kuondoa tofauti zinazojitokeza, kuwepo na utaratibu mzuri wa usuluhishi, na Watanzania tujitajidi kuishi kwa amani, mshikamano na upendo.
Taarifa muhimu ya mapato na matumizi ya Jumuiya kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2009/2010 iliwasilishwa. Wajumbe walitoa hati safi kwa mahesabu hayo na kusisitiza jitihada ziongozwe kuweza kutunisha zaidi mfuko wa Jumuiya hususan kwenye makusanyo ya ada mbalimbali.
Aidha kwenye mkutano huo viongozi wa Jumuiya waliwasilisha utaratibu mpya utakaotumika kwa wanachama watakaopatwa na matatizo kuomba msaada wa Jumuiya. Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya, Bw. Ebby Senkoro aliwasilishwa pendekezo hilo kwa wajumbe na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu faida zake. Uongozi umesisitiza kwamba Watanzania ambao ni wanachama wa Jumuiya na wanaotimiza wajibu wao kama wanachama ikiwa ni pamoja na kulipa ada na michango mbalimbali ya Jumuiya wataendelea kupatiwa msaada wa hali na mali kwa mujibu wa Katiba.
Mkutano huo pia ulijadili kuhusu kutoa msaada kwa wale waliofikwa na majanga kule nyumbani.
Mwenyekiti wa Jumuiya pia aliwakaribisha na kuwatambulisha Bw. Chacha na Bw. Viktor waliokuwa ni wageni kwenye mkutano huo na kuwapa fursa kuwasalimia wananchi. Bw. Chacha ni katibu mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Watanzania huko Washington Metro nchini Marekani
No comments: