Monday, March 28, 2011

Tanzanite SocietyMCHANGO KWA WALIOPATWA NA MAAFA SEHEMU ZA MIYAGI, IWATE, IBARAKI, FUKUSHIMA - JAPANNdugu Wanajumuiya na Watanzania Wote Mnaoishi Japan, Waliowahi kuishi Japan na wengine wote ambao wameguswa na janga hili kwa namna moja au nyingine. Naomba nianze kwa kutoa mfano mdogo :


Fikiria kuwa umesafiri ili kutimiza baadhi ya malengo yako katika maisha ukafika sehemu ukakaribishwa na mtu usiyemjua, akakuruhusu kuishi kwenye nyumba yake pamoja na familia yake mpaka utakapokamilisha malengo yako. Ukiwa hapo nyumba inashika moto na kuunguza vibaya mali pamoja na sehemu kubwa ya familia ya mwenyeji wako, na wengine kukimbilia sehemu ambazo wanadhani watapata hifadhi. Bahati nzuri umesalimika, je utakimbia haraka kurudi ulikotoka? utakaa pembeni kumuangalia akihangaika? au utajaribu kuokoa japo kitu kidogo utakachoweza kukifikia? Kwa wale ambao walisha kamilisha malengo yao na kuondoka.


Hili janga limetokea na umepata taarifa ikiwa pamoja na kuona mwenyewe kwenye vyombo vya habari. Je utakaa kimya kwa vile ulishakamilisha malengo na kuondoka? Tumo kwenye wiki ya tatu tangu kutokea kwa janga kubwa la tetemeko la ardhi pamoja na Tsunami iliyozoa maisha ya maelfu ya binadamu wenzetu na kuwaacha wengine wakikabiliana na matatizo mbali-mbali.


Miongoni mwao wapo watoto wachanga, Wazee, Watu wasiojiweza, kina mama na watu wengine wengi. “Mwenyeji wetu ameunguliwa na nyumba, sehemu kubwa ya familia yake imepoteza maisha, mali zimeteketea nk.


Moto unaendelea kuwaka…..Fukushima Power Plant, ... Ni vigumu kuamini kuwa Yen 300 au Yen 500 uliyonayo mfukoni inaweza kusaidia kurefusha uhai wa mtoto mdogo kwa kupata maji ya chupa ambayo yatamsaidia mtoto huyu japo kwa siku nzima. Hawa ni watu ambao walikuwa na maisha yao ya kawaida tu, mpaka siku ya dhoruba waliamka na kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Ni zile dakika zisizozidi 30, ndizo zilizobadili maisha yao yote.


Ni kawaida katika maadili yetu kujumuika na ndugu, marafiki, wenzetu mashuleni/ Vyuoni /makazini, na hata majirani zetu wanapokuwa na sherehe mbali-mbali, na pia wanapofikwa na huzuni. Mara nyingi hasa tunapotoa pole kwa wenzetu wanafikwa na huzuni hutoa tulichonacho (hatuwekeani viwango).


Tumeshaonyesha mfano siku za nyuma kwa kuwachangia wenzetu walipatwa na maafa huko Morogoro, bahati mbaya tulishindwa kuji-organise mapema kuchangia wenzetu wa Gongo la Mboto, kutokana na baadhi yetu kuwa kwenye safari za kikazi. Tunawashukuru wote wanaotumia muda wao mwingi kwa ajili ya kutafuta habari na kutuletea taarifa za hali inavyoendelea kupitia humu mtandaoni. Hawa ni pamoja na Ubalozi wetu, na wachangiaji binafsi.


Tunawashukuru sana wenzetu walionza kuonyesha mioyo ya huruma kwa kujitolea kuchangia damu. Orodha hii bado ipo wazi kwa wale watakaopenda kuongeza majina yao na shughuli hii itasimamiwa na ubalozi wetu kama ilivyoelezwa kwenye jumbe za awali.


Kwa niaba ya Jumuiya yetu natumia fursa hii kuwaomba wote wanaoona ipo haja ya kusaidia japo kununua maji ya kunywa ya mtoto mchanga kwa siku. Nawaomba kujitolea kwa hali na mali kuwasaidia jirani zetu, wenyeji wetu katika kupunguza makali ya matatizo waliyoyapata, japo kwa kiasi fulani.


Wito huu tunautoa kwa yeyote yule anayeona ameguswa na hali iliyotokea. Unaweza kuwa mwana-jumuiya au si mwanajumuiya., unaishi Japan au nje ya Japan, hata kama haumo kwenye makundi niliyoyataja hapa juu, lakini umeguswa na hali hii, unakaribishwa kutoa mchango wako.


Tutapokea michango yote kupitia akaunti ya Jumuiya na kuiwasilisha kunakohusika baada ya kuitolea taarifa. Ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa michango hii, tutaandika jina la kila anayechanga na kiasi alichochanga. Kwa yeyote ambaye atashauri jina lake lisitokee/ lisionekane kwenye ripoti, tutafuata maagizo yake.


Tunaweza kutoa namba za utambulisho ambazo mtoaji anaweza kuoanisha na kiwango alichotoa kitakachoonekana kwenye ripoti. Naomba nianzishe mchango huu kwa kutoa nilichonacho (Yen 20,000). Kiwango hiki hakimaanishi kuwa ni kiwango cha chini au cha juu,


“KILA MMOJA YUKO HURU KUTOA ALICHONACHO AU ANACHOPANGA KUTOA.” MICHANGO HII IMEANZA KUKUSANYWA LEO TAREHE 27/MACHI/2011, TUTAENDELEA KUKUSANYA HADI JUMANNE IJAYO, TAREHE 05/APRILI/2011.


Minna sama gokyouryoku o onegaishimasu.


NJENGA, Rashid MBA Makamu Mwenyekiti Jumuiya ya Watanzania Wanaoishi Nchini Japan


Zifuatazo ni Benki Akaunti pamoja na daftari ambazo zitatumika kupokea Michango. =================================


ACC. NAME: Tanzanite Society


REPRESENTATIVE:


Simba Ally Yahaya


ACC No.: 7916169


BRACH NAME: Kunitachi BRANCH


No.: 666 BANK NAME: Mitsui Sumitomo==============================


Kwa wale wanaoishi maeneo ya Sagamihara mnaweza kujiandikisha na kukabidhi michango yenu kwa Ndugu Gwakisa. Wale watakaoweza kufika kwa Ndugu Prosper Sugai, kutakuwa na daftari pia mnaloweza kujiandikisha.

1 comment:

emu-three said...

Huku bongo tunachoweza kusema ni `poleni sana na maafa hayo tupo pamoja!